Monday, September 10, 2012

IKIZU High school yachomwa moto

.

WANAFUNZI 100 wa Kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Ikizu inayomilikiwa na kanisa la Wasabato iliyoko wilayani Bunda hawana mahali pa kulala baada ya mabweni yao mawili kuchomwa moto na watu wasiofahamika.

Mkuu wa wilaya ya Bunda Joshua Mirumbe amewaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake kuwa mabweni hayo yaliungua usiku wa Sep 8 mwaka huu majira ya saa 3 usiku.

Alisema kuwa  tukio hilo limetokea wakati wanafunzi wakiwa wanajisomea madarasani  ambapo mwanafunzi mmoja aligundua moto uliokuwa ukiwaka katika mabweni hayona ndipo alipotoa taarifa kwa viongozi wa shule hiyo.

Mirumbe  alisema kuwa baada ya uongozi kuona hali hiyo ulitoa taarifa polisi na maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuomba msaada katika kikosi cha zimamoto mkoa ambao walifika eneo la tukio na kuanza kuzima moto huo kwa kushirikiana  na wanafunzi pamoja  na wanakijiji wa eneo hilo.

Alifafanua kuwa hadi sasa chanzo cha moto huo hakijajulikana na kwamba baada ya tukio hilo kutokea kamati ya ulinzi na usalama ikongozwa na yeye mwenyewe ilifika eneo la tukio na kufanya kikao na uongozi wa shule hiyo ambapo pamoja na mambo mengine wameunda tume ya uchunguzi ili kubaini chanzo cha moto huo shuleni hapo.

“ Tumeunda tume ili kubaini tatizo hilo ambayo itaongozwa na mkuu wa upelelezi wa wilaya,afisa usalama wa wilaya,mshauri wa mgambo,mkuu wa kikosi cha zimamoto mkoa,wamiliki wa shule,uongozi wa kijiji na katibu tawala wa wilaya ambaye ndiye atakuwa katibu wa tume hiyo ambapo itafanya kazi kwa muda wa siku saba’’alisema Mirumbe.

Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya ametoa wito kwa wananchi,taasisi na watu binafsi kuchangia chochote walichonacho ili mabweni hayo yaweze kujengwa upya na wanafunzi hao waliounguliwa vitu vyao  waweze kununuliwa kwani wanafunzi hao kwa sasa hawatarudi nyumbani bali wataendelea kuwa hapo shuleni kwani mtihani imekaribia ambapo ameuagiza uongozi wa shule kuwapa taarifa wazazi ili waje wawasalimie watoto wao.

Aliongeza kuwa mkoa na wilaya vinaangalia jinsi ya kuwasadia wanafunzi hao ingawa tayari  mashirika ya kanisa hilo la wasabato wameshatoa baadhi ya misaada kwa wanafunzi hao ili waendelee kusoma.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya amekanusha taarifa zilizotolewa na radio free Afrika katika kipindi chake cha matukio kuwa chanzo cha kuungua mabweni hayo ni kutokana na hitirafu ya umeme jambo ambalo alisema kuwa siyo sahihi na ndo maana wameunda tume ili iweze kupata ukweli..
Baadhi ya wanafunzi walizungumza na gazeti hili jana wameonyesha hofu kutokana na kuwepo kwa matukio ya kuchomwa shule za sekondari mara kwa mara hapa nchini ambapo wamedai hata kusoma kwao sasa kutakuwa kwa shida.

Taarifa za awali zilizopatikana shuleni hapo zinaonyesha kuwa hasara ya vitu vyote vilivyoungua katika mabweni hayo ni kiasi cha shilingi million 19.317.000 ikiwa ni pamoja na majengo yenyewe.

Hii ni mara ya pili kwa shule hiyo ambapo mwaka 2006 wanafunzi wa shule hiyo walisadikiwa kuchoma jengo la utawala la shule hiyo baada ya kile kilichodaiwa kuwa wamenyimwa wali shuleni hao.

Mwisho


No comments:

Post a Comment

Comments System

disqus

Disqus Shortname

msora

Popular Posts

Header Ads

ad