NA Berensi Alikadi-Musoma
CHAMA cha waandishi wa habari mkoani Mara {MRPC] kimemfukuza uanachama wa chama hicho mwandishi wa habari wa radio Free Afrika mkoani Mara Maxmilian Ngesi baada ya kukiuka makubalino ya chama hicho yaliyofikiwa juzi ya kutoandika kabisa habari za jeshi la polisi mkoani humo.
Akizungumza na gazeti hili jana asubuhi mwenyekiti wa chama hicho Emmanuel Bwimbo alisema kuwa Ngesi amekiuka makubaliano ya waandishi wenzake na chama kwa ujumla baada ya kusikika akitangaza habari za jeshi la polisi kuhusiana na ajari ya kipanya iliyotokea juzi katika kijiji cha Muriaza wilayani Butiama ambapo alimkariri kamanda wa polisi wa mkoa huo.
Bwimbo amesema kuwa kitendo hicho kinaonyesha jinsi mwandishi huyo alivyokishika chama hicho miguu na kuwa saliti wenzao ambao walikubaliana kwa pamoja juzi katika tamko lao walilotoa ofisini hapo baada ya kuzuiwa wasiandamane kulaani mauaji ya mwenzetu Daudi Mwangosi aliyeuwa na polisi hivi karibuni.
Alisema kuwa yeye kama mwanachama alitakiwa kutii maamuzi ya chama na tamko la chama hilo maana ni tamko ambalo limetamkwa na wananchama na siyo kwa mkoa wa Mara tu lakini pia baadhi ya mikoa imetoa matamko na misimamo hiyo lakini cha kushangaza yeye amekaidi na kwenda kujipendekeza kwa polisi.
‘’Kwakweli huyu mzee ni wa ajabu sisi kama chama tumetoa tamko na vyombo vimetangaza sasa tunashangaa kusikia leo asubuhi anatangaza habari kwa kumkariri RPC sasa kamasi unafiki ni nini mimi naona amezeeka ni bora aache kazi aendelee na kazi yake ya uenezi wa CCM’’alisema Bwimbo.
Alifafanua kuwa kamwe chama hicho hakiwezi kuvumilia mwandishi atakaye kiuka agizo hilo hivyo Ngesi atakuwa mfano kwa waandishi wale ambao wanatakwenda kwenda kujikomba na kuandika habari za polisi hivyo uamuzi pekee wa kumfukuza uanachama ni sahihi kabisa na kwamba chama hicho hakitamrudishia tena uanachama wake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wadau wa habari wa mkoa wa Mara na wilaya za Bunda,Tarime na Serengeti wameonyeshwa kusikitisha sana na kitendo cha mwandishi huyo cha kuwasaliti waandishi wenzake ambapo wamedai kuwa mwandishi huyo hafai tena kuwa mwanachama wa chama hicho.
Nao baadhi ya waandishi habari wa mkoa wa Mara wameonyesha kukerwa na tabia ya mwandishi huyo ya kukiuka makubalino na wenzake ambapo wamedai kuwa amewadhalilisha hivyo hawako tayari kufanya kazi naye na kwamba hata kama akipata matatizo hawako tayari kufika kwake.
Juzi waandishi wa habari walifanya maandamano nchi nzima wakilaani mauaji ya mwandishi mwenzao Daudi Mwangosi ambapo kwa mkoa wa Mara maandamano hayo yaliuzuiwa na polisi hali iliyofanya chama cha waandishi wa habari kukataa kuandika habari za jeshi hilo mkoani Mara.
MWISHO
No comments:
Post a Comment