Friday, August 31, 2012

Mbuyu Twite usipime Dar


na Dina Ismail

Aidha, fulana zenye rangi ya kijani na njano zilizoandikwa jina la Twite, ziliuzwa kwa wingi uwanjani hapo kwa kati ya sh 10,000 hadi 15,000.
HATIMAYE mzizi wa fitina umekatwa, beki wa kimataifa wa Yanga, Mbuyu Twite ametua rasmi nchini na kupokewa kwa kishindo na shangwe za aina yake, hivyo kuhitimisha filamu ya ujio wake.
Twite ambaye usajili wake umezua gumzo kutokana na kujisajili pia kwa mahasimu wao wa jadi nchini, Simba, alitua Uwanja wa kimataifa wa JK Nyerere majira ya saa 10 alasiri na ndege ya Rwanda Air, akitokea mjini Kigali.
Hata hivyo, Simba ambayo ilidai ingemkamata nyota huyo baada tu ya kutua nchini kwamba ina taarifa ya kumsaka nyota huyo (RB), aliyekuwa akikipiga APR ya Rwanda kwa mkopo akitokea FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ilishindwa kufanya hivyo.
Simba ilitangaza kumkamata Twite kwa madai ya kuwatapeli dola 30,000 za Marekani ilizompa kama dau la usajili, kabla ya Yanga kumuongeza dau la dola 50,000 na hatimaye kufanikiwa kunasa saini yake.
Mara baada ya kutokeza katika lango la watu mashuhuri uwanjani hapo, Twite alivalishwa jezi namba 4 ya Yanga, ambayo nyuma iliandikwa jina la Mwenyekiti wa Simba, Rage (Alhaj Ismail Aden Rage).
Akizungumza uwanjani hapo, Twite alisema amekuja Tanzania kwa ajili ya kuitumikia Yanga na si kingine, hivyo mashabiki wasubiri mambo mazuri kutoka kwake.
Hata hivyo, Twite aligoma kuzungumzia hatua yake ya kusaini Simba na baadaye Yanga kwa madai kwamba ni habari ndefu na watu wanazungumza sana, hivyo ni kulipotezea tu.
“Siwezi kulizungumzia suala hilo (kusaini Simba), kwani maneno mengi yanasema na yataendelea kusemwa,” alisema Twite.
Katika mapokezi hayo, umati mkubwa wa mashabiki wa Yanga, ulifurika uwanjani hapo kwa lengo la kumlaki nyota huyo ambako walikuwa wakifurahi kwa kuimba kucheza na kupiga matarumbeta.
Kama hiyo haitoshi, mashabiki hao ambao wakiwa wamevalia jezi zilizoandikwa ‘Twite,’ walionesha mapenzi yao kwa mchezaji huyo, baada ya kumbeba kwa mita kadhaa baada ya kutoka nje ya uwanja kabla ya kumuacha na kupanda gari la klabu.
Aidha, fulana zenye rangi ya kijani na njano zilizoandikwa jina la Twite, ziliuzwa kwa wingi uwanjani hapo kwa kati ya sh 10,000 hadi 15,000.
Katika hatua nyingine, mashabiki hao wa Yanga, walimchania fulana ya Simba kijana mmoja ambaye alifika uwanjani hapo kwa shughuli zake binafsi.


No comments:

Post a Comment

Comments System

disqus

Disqus Shortname

msora

Popular Posts

Header Ads

ad