JESHI la polisi mkoani Mara linatarajia kumfikisha mahakamani mtu mmoja aitwaye Issa Ibrahimu 30 mkazi wa kamunyonge katika manspaa ya Musoma kwa kosa la kumshikia panga karani wa Sensa
Akiongea na waandishi wa habari jana ofisini kwake kwa niaba ya kamanda wa polisi,mkuu wa upelelezi wa mkoa wa Mara Emanuel Lukula alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Agost 26 mwaka huu baada ya kumshikia panga karani wa Sensa na kumfukuza huku akidai kuwa imani ya dini yake ya kiislam haimuruhusu yeye pamoja na familia yake kuhesabiwa.
Lukula alisema kuwa baada ya karani huyo kupata vitisho hivyo alienda hadi katika kituo cha polisi ambapo alitoa taarifa na ndipo polisi walienda na kumakamata na kumfungulia mashitaka na kwamba upelelezi ukikamilika watamfikisha mahakamani ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabiri.
Kaimu kamanda huyo alisema kuwa hadi jana ofisi yake ilikuwa haijapata taarifa kuhusu watu wengeine ambao wanatuhumiwa kuvuruga zoezi la Sensa katika mkoa mzima wa Mara na hivyo akatoa wito kwa wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa makarani wa Sensa ambao wanaendelea na zoezi hilo hivi sasa.
‘’Kwakweli hatujapokea taarifa nyingine ikiacha hii na nyingine kule wilayani Bunda ambako alikamatwa mwenyekiti wa kitongoji ambaye tayari ameshafikishwa mahakamani kwa kosa kama hili kwa hiyo ni matumaini yetu kuwa zoezi litaenda vizuri’’alisema Lukula.
Aliongeza kuwa jeshi la polisi mkoani humo halitamuea aibu mtu yeyote atakayejaribu kuvuruga zoezi la Sensa ya watu na makazi linaloendelea hivi sasa na kwamba atakayejaribu atakamatwa anafikishwa mahakamani kwa mjibu wa sheria ya Takwimu.
No comments:
Post a Comment