Friday, September 14, 2012


DDH Bunda hawana X-Ray
Na Tezra Lusenga Bunda;
Septe 13, 2012;

HOSPTAL teule ya wilaya ya Bunda mkoani Mara haina huduma ya mashine ya X-Ray kwa zaidi ya miezi sita ambapo hali hiyo imekuwa kisababisha kero kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.

Hayo yameleezwa leo na mganga mkuu wa wilaya ya Bunda, Dk. Riner Kapinga, kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichoketi katika ukumbi wa halmashari mjini Bunda.

Dk. Kapinga amesema kuwa X-Ray iliyokuwepo katika hospitali hiyo iliharibika na kwamba kwa kipindi hicho chote wagonjwa wamekuwa wakitaabika sana na kulazimika kupelekwa katika hospitali za misheni Kibara, hospitali ya mkoa wa Mara mjini Musoma na katika hospitali ya rufaa Bugando ya jijijini Mwanza.

Amesema kuwa kufuatia hali hiyo halmashauri ya wilaya ya Bunda, imetoa kiasi cha sh. Milioni mbili kwa ajili ya kuleta mafundi wa kampuni Philips, iliyoingia mkataba na wizara ya afya ili waweze kuangalia uwezekano wa kuitengeneza X-Ray hiyo.

Wakichangia kwenye kikao hicho, madiwani wamesema kuwa hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maji ya kutosha hali ambayo imekuwa ikisababisha kukithiri kwa uchafu hospitalini hapo.

Diwani wa kata ya Balili ambako ndiko iliko hospitali hiyo, Bw. Georges Miyawa, amesema kuwa hupungufu huo wa maji umesababisha baadhi ya vyoo katika hospitali hiyo kuziba, hali ambayo imesababisha uchafu kutiririka hovyo.

Aidha, mhandisi wa maji katika mji mdogo wa Bunda, Injinia Idd Swai, amesema kuwa maji katika mji wa Bunda yamekuwa yakitoka kwa mgao na kwamba upungufu wa maji katika hospitali hiyo ni kutokana na tanki moja la maji kupasuka.

Injinia Swai ameutaka uongozi wa hospitali hiyo kutengeneza tanki hilo ili wanapowasukumia maji waweze kuyahifadhi katika mantaki yote matatu yaliyoko hospitalini hapo, ili wanapopitisha mgao wawe na akiba ya kutosha.

Mwisho

No comments:

Post a Comment

Comments System

disqus

Disqus Shortname

msora

Popular Posts

Header Ads

ad