Friday, July 19, 2013

MOSHI WA KIWANDA HATARI KWA WAALIMU NA.WANAFUNZI.


NA Berensi Alikadi Musoma.
20/7/2013
WAALIMU na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Bweri iliyoko katika manispaa ya Musoma wamesema moshi mwingi unaotoka katika kiwanda cha nguo cha Mutex ni hatari kwa afya yao na kwamba umekuwa ukiwapa wakati mgumu wa kufundisha shuleni hapo.
Waalimu hao walitoa kilio chao hicho jana kwa mbunge wa jimbo la Musoma Vicent Nyerere kwa tiketi ya Chadema wakati alipotembelea shule hiyo na kisha kuongea na waalimu na wanafunzi.
Walisema kuwa kwa muda mrefu sasa moshi mwingi unaotoka katika kiwanda hicho cha nguo umekuwa ukiwaathiri wao pamoja na wanafunzi wakati wa masomo kwani umekuwa ukiingia madarani jambo ambalo sasa limeonekana kuwa sugu na kwamba wao licha ya kulalamika lakini hawaoni jitihada zozote zinazofanyika na uongozi wa manispaa ili kuzuia moshi huo.
‘’Kwakweli mbunge huu moshi unatuumiza sana sisi waalimu tunafundisha kwa shida na hata watoto wetu wanasoma kwa shida sana leo kwa vile umetutembelea tunaomba tukueleze kabisa kero hii ili uweze kuona namna ya kutusaidia’’alisema Mwalimu Madede
Pamoja na kero hiyo pia waalimu hao walimwambia mbunge huyo kuwa kumekuwepo na tatizo la vikundi vya Jamaica Mokas ambavyo vimekuwa ni tishio kwa waalimu na kwamba imefikia hatua mpaka vinakuja shuleni hapo na kuvizia waalimu jambo ambalo ni hatari kwao kwani shule yao haina uzio.
Aidha kero nyingine waliyomwambia mbunge huyo ni pamoja na wao kunywa maji machafu ambayo hayakuchujwa wala kuwekewa dawa na kwamba maji hayo yako kwenye eneo la mkondo wa kiwanda cha nguo kinapomwaga maji machafu jambo ambalo walidai kuwa afya zao ziko hatalini.
Akijibu hoja hizo mbunge huyo alisema kuwa suala la kiwanda cha Mutex kutoa moshi ni hatari ambapo aliahidi kwenda yeye mwenyewe kiwandani hapo ili aweze kuonana na mhusika.
Kuhusu kero ya maji aliwahakikishia waalimu hao kuwa atajitahidi kuonana na uongozi wa Muwasa ili kufahamu ni kwa nini hawaweki dawa katika maji lakini pia akawapa matumaini kuwa upo mradi mkubwa wa maji unaojengwa eneo la makoko na kwamba unatarajia kukamilikwa mwakani ambapo wananchi wa Musoma sasa hawatakuwa tena na shida ya maji.
Mbunge huyo pia alitumia fursa hiyo kuwaasa wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii na kuachana na kujiunga na vikundi viovu kwani wazazi wao wanajitahidi kuwalipia karo hivyo njia pekee ya kujinasua katika umasikini ni elimu na wala si jambo linguine.
Akiwa katika shule hiyo mbunge huyo pia aliweza kukagua jengo la maabara ya kisasa ambalo limejengwa kwa gharama ya kiasi cha shilingi pesa ambayo imetokana na mfuko wa jimbo.
Mwisho

No comments:

Post a Comment

Comments System

disqus

Disqus Shortname

msora

Popular Posts

Header Ads

ad