Ramadhani Singano ‘Messi’ (katikati) akizungumza na waandishi wa habari maara baada ya kikao chao na TFF kumalizika
Baada ya uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutoa uamuzi juu ya sakata la kimkataba lililokuwa linamhusu winga Ramadhani Singano na klabu yake ya Simba ambapo TFF imeivunja mikataba yote miwili, wa Singano na wa Simba huku ikiwashauri Simba SC kukaa meza moja na Singano ili kujadiliana upya suala la mkataba mwingine kwa ajili ya msimu mwingine.
Singano amesema kuwa, anamshukuru Mungu kwa mikataba yote kuvunjwa na hiyo inamaanisha yeye ni mchezaji huru huku akisema amepata fundisho kubwa juu ya maswala ya mikataba na kuwashauri wachezaji wengine kutafuta watu wa kuwasaidia hasa pale inapokuja suala la kusaini mikataba ili kuzitumikia timu zinazohitaji saini zao.
“Wamesema (TFF) mikataba yote imefutwa kwahiyo mimi nikae chini na Simba tukubaliane upya kwasababu mimi kwasasa ni mchezaji huru, na kama ikitokea tumeshindwana basi mimi ntaongea na timu nyingine. Kikubwa tukae chini tuzungumze kama na wao bado wana nia na mimi”, amesema Singano.
“Ianabidi sasahivi ndiyo wanipe ‘proposal’ yao ya mkataba niiangalie halafu na mimi niingize vitu vyangu, waulete huo mkataba wao mpya niusome kwanza lakini kikubwa sio kukomoana. Mimi namshukuru Mungu kwakuwa wao wenyewe wamekubali kwamba hapa kuna utata na kukubali mikataba yote ifutwe tuanze upya, namshukuru sana Mungu kwa hili”, Singano alisisitiza.
“Nimejifunza kitu kimoja kwamba yani si kila kitu unachokiona ndo ukiamini hichohicho, inabidi ukione na ukifanyie utafiti. Nawashauri wachezaji wengine kabla ya kusaini mikataba na timu zao wasikose watu wa kuwaongoza, maana utakapokwama utaongozwa na mtu huyo, lakini ukikosa utahangaika sana”, ameshauri Singano.
Kwa upande wa Simba SC kupitia kwa afisa habari wao Hajji Manara wamesema, kesho watafanya kikao cha kamati ya utendaji. Moja ya ajenda zao ni kujadili kuhusu suala la Singano na watatoa kauli ya timu baada ya kikao hicho kukamilika na kupata majibu juu ya jambo hilo.