Wednesday, November 10, 2010

MWALIMU NYERERE NURU YA WANYONGE ILIYOZIMIKA

MWALIMU NYERERE NURU YA WANYONGE ILIYOZIMIKA
NA Berensi Alikadi-Bunda

BABA wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa Aprili 1922, katika eneo la Mwitongo, Muhunda kijijini Butiama.
Baba yake, Nyerere Burito, alikuwa Chifu wa kabila dogo la Wazanaki, na alifariki dunia mwaka 1942 na kuzikwa hapo hapo kijijini Butiama.
Inakisiwa kwamba, mnamo mwaka 1800, kulikuwa na kaya 80 tu za Wazanaki; mama yake aliitwa Mgaya Nyang’ombe, alifariki dunia mwaka 1997.
Kama ilivyokuwa kwa watoto wengine, Kambarage alikuwa katika maisha ya dhiki, ingawa alikuwa mtoto wa chifu, alifanya kazi ya uchungaji wa mifugo na mara kadhaa alimsaidia mama yake kazi za kilimo.
Mwalimu Nyerere alianza kusoma akiwa na umnri wa miaka 12, katika Shule ya Msingi Mwisenge iliyopo Musoma mjini, ingawa kuna habari kwamba Chifu Nyerere hakutaka Kambarage asome.
Lakini baadaye, ilikuja kubainika kuwa mzee huyo ndiye aliyeacha wosia kwa Wanzagi Nyerere (kaka yake Mwalimu), akimtaka ahakikishe kwamba Kambarage anasoma kwa bidii.
Wanafamilia wanasema kwamba, Chifu Nyerere alitoa wosia huo siku chache tu kabla ya kifo chake. Naye Wanzagi, ambaye baada ya kifo cha baba yake aliteuliwa kuwa chifu, alitekeleza wosia wa baba yake huyo. Chifu alitoa msaada kwa Kambarage, uliomwezesha kusoma na hatimaye kupata mafanikio makubwa.
Baada ya kutoka Mwisenge, alichaguliwa kwenda kupata masomo ya sekondari mkoani Tabora, katika shule iliyokuwa ya watoto wa machifu. Hapo Tabora alifanya vizuri na kuchaguliwa kujiunga na masomo ya juu, katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda.
Kutoka huko, alirejea Tabora kufundisha katika Shule ya St. Mary. Mwaka 1949 alijiunga na Chuo Kikuu cha Edinburgh, Scotland, akisomea shahada ya uzamili (MA) katika masuala ya historia na uchumi, aliyohitimu mwaka 1952.
Baada ya kutoka huko, alikwenda kufundisha tena katika Shule ya Mtakatifu Francis, Pugu, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Akiwa Pugu, alianza kujihusisha kwa bidii zaidi katika masuala ya siasa, wakati mwingine alisema, alipenda sana kuwa daktari wa binadamu, lakini baadaye aliona bora awe mwalimu, ili awatoe wengi gizani.
Baada ya kufanya kazi ya kufundisha kwa miaka kadhaa, aliona ajiingize moja kwa moja kwenye siasa, ili aendeshe mapambano ya kuwaondoa wakoloni, kwa msingi huo, akiwa mwalimu katika Shule ya Mtakatifu Francis, mwaka 1953 aliweza kuwa mwanachama wa chama kilichokuwa kikiitwa TAA, yaani Tanganyika African Association.
Hata hivyo, awali chama hicho hakikujitambulisha moja kwa moja kisiasa kwa wananchi na serikali ya kikoloni. Mwalimu Nyerere alikuwa mwenyekiti wa chama hicho.
Mwaka mmoja baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TAA, ilipofika Julai 7, 1954, chama hicho kilibadilisha jina na kuitwa Tanganyika African National Union (TANU), na Mwalimu Nyerere akawa rais wake wa kwanza.
Malengo ya chama hicho, kama yalivyotangazwa na Mwalimu Nyerere, yalikuwa kuifanya Tanganyika iwe nchi huru. Pia Mwalimu akiwa na TANU alihakikisha kwamba chama hicho kinajitahidi kujenga nchi isiyokuwa na ukabila wala ubaguzi wa aina yoyote ile.
Mnamo mwaka 1955, Mwalimu Nyerere alipata wakati mgumu kutoka kwa serikali ya kikoloni, kwa kuwa wakati huo wafanyakazi wa serikali hawakuruhusiwa hata kidogo kujihusisha na masuala ya siasa, hivyo alitakiwa achague moja, kati ya siasa na ualimu. Yeye akaamua kuchagua siasa, na huo ukawa ndio mwisho wake wa kuajiriwa serikalini kama mwalimu. Lakini akabaki na jina lake la Mwalimu hata leo.
Julai 1957, Mwalimu Nyerere aliteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria (LEGCO), lakini alijiuzulu nafasi hiyo Desemba mwaka huo huo. Hata hivyo, ikumbukwe kwamba, Mwalimu alipata kuhutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa, akiwa katika juhudi za kutaka Tanganyika iwe huru kutoka katika makucha ya ukoloni wa Kiingereza.
Mwaka 1958, alipinga vikali mpango wa serikali ya kikoloni, wa kufanya uchaguzi wa wajumbe wa LEGCO. Alipinga mpango wa wakoloni kutoa theluthi mbili ya viti vyote kwa Wazungu na Waasia. Mabadiliko yalipofanywa, TANU ilipata kura nyingi na Mwalimu Nyerere akawa mmoja wa wajumbe wa baraza hilo.
Hali kama hiyo ilijitokeza tena katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1960, aliposhinda na kutangazwa kuwa Waziri Mkuu. Mei Mosi 1960, aliapishwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika, chini ya Serikali ya Madaraka, na Desemba 9, 1961, nchi ilipata uhuru, mwenyewe akaendelea kuwa Waziri Mkuu.
Miezi sita baadaye, alijiuzulu nafasi hiyo, kwa maelezo kwamba alitaka kwenda kuiimarisha TANU, na nafasi yake ikachukuliwa na Rashid Mfaume Kawawa. Mwaka 1962 Mwalimu Nyerere aliteuliwa na TANU kuwa mgombea urais. Katika uchaguzi huo, Mwalimu alipata asilimia 97 ya kura zote.
Desemba 9, aliapishwa kuwa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika, Ikulu ikawa makazi yake rasmi kama rais wa nchi.
Jitihada za Mwalimu Nyerere hazikuishia kwenye uhuru wa Tanganyika tu, bali mwaka 1964 alifanya kazi kubwa ya kuiunganisha Tanganyika na Zanzibar, akishirikiana na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, ambaye pia alijua umuhimu wa kuwapo Muungano. Ndipo ikazaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aprili 26, 1964.
Hata hivyo, mwaka huo huo, yalitokea maasi ya baadhi ya askari wa jeshi lililorithiwa kutoka kwa wakoloni. Jeshi hilo lilivunjwa na kuundwa jeshi jipya – Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Mwalimu Nyerere mwenyewe akiwa Amiri Jeshi Mkuu wa kwanza.
Wimbi la mabadiliko chini ya uongozi wake liliendelea kujitokeza. Mwaka 1967 alitangaza Azimio la Arusha. Kutokana na azimio hilo, mali nyingi zilitaifishwa, baadhi zikiwa ni majumba, mashamba, viwanda, kampuni binafsi na kuhakikisha kwamba njia kuu za uchumi zinamilikiwa na umma.
Azimio hilo ndilo lililotoa mwelekeo wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, ndoto kubwa kabisa ya Mwalimu. Aliamini sana katika ujamaa na kujitegemea, na kwamba siasa hiyo isingefanikiwa kama watu wangeendelea kuishi mbalimbali.
Mwaka 1970 Tanzania ilikumbwa na tatizo kubwa la njaa. Kukawa na kupanda kwa bei ya mafuta na bidhaa nyingine nyingi, hali iliyouweka uchumi wa Tanzania katika hali mbaya. Ilitangazwa vita dhidi ya tatizo hilo.
Ilikuja kutokezea kwamba, baadhi ya watu walijilimbikizia mali nyingi kinyume cha matakwa ya Mwalimu na sera za nchi, ikaanzishwa operesheni dhidi ya wahujumu uchumi. Kiongozi wa mapambano hayo, alikuwa Waziri Mkuu wa wakati huo, hayati Edward Moringe Sokoine, kipenzi cha Mwalimu na Watanzania wote.
Kwa msingi huo, mwaka 1974 alitangaza Operesheni ya Vijiji vya Ujamaa. Watu walihamia kwenye vijiji vipya vya ujamaa kwa hiari yao, lakini waliopinga walihamishwa kwa nguvu. Kulikuwapo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu utekelezwaji wa mpango huo, licha ya nia yake nzuri.
Kufikia mwaka 1977, karibu asilimia 80 ya Watanzania wote walikuwa wakiishi katika vijiji vya ujamaa, huku wakiwa wameboreshewa huduma muhimu kama elimu, maji na afya – huduma za jamii, ingawa hapakuwapo mabadiliko makubwa sana kama yalivyokuwa matarajio yake.
Mwaka 1977 pia, Mwalimu Nyerere alitimiza ndoto yake ya kuviunganisha vyama vya TANU na Afro Shirazi Party (ASP). Hiyo ilikuwa Februari 5, 1977. Vyama hivyo viliungana na kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akiwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mwalimu alitangaza vita dhidi ya nduli Idi Amin Dada wa Uganda mwaka 1978, aliyekuwa amevamia na kuchukua kipande cha Tanzania, akidai ni chake. Mwaka 1979 ulishuhudia majeshi ya Uganda yakiwa yameshindwa vibaya katika vita hiyo, nduli mwenyewe akang’olewa na Uganda mpya ikaanza kujengwa.
Baada ya kuongoza kwa miaka mingi, hatimaye Mwalimu Nyerere alitangaza rasmi kustaafu urais, na alitimiza ahadi hiyo mwaka 1985, akimwachia jahazi mteule wake, Ali Hassan Mwinyi.
Bado Tanzania iliweza kujivunia rekodi nzuri ya kutokomeza ujinga. Hadi Mwalimu Nyerere anang’atuka mwaka 1985, zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania walikuwa wanajua kusoma na kuandika.
Licha ya kustaafu urais, aliendelea na uenyekiti wa CCM hadi alipoamua pia kujing’atua, mwaka 1990 na kumkabidhi Mwinyi. Hata hivyo, aliendelea kuwa kinara wa siasa za ndani na nje ya nchi, akipata sifa kubwa kimataifa. Aliendelea na uenyekiti wa nchi za kusini hadi mauti yalipomfika.
Mwalimu alikuwa mstari wa mbele kupinga mfumo mbaya wa uchumi kati ya nchi tajiri na maskini, alilalamikia pia fursa finyu na madeni makubwa kwa nchi maskini kama Tanzania. Alipigania madeni hayo yafutwe, ili fedha hizo zitumike kuandaa na kuendeleza huduma za jamii kwa mamilioni ya watu katika nchi maskini.
Hadi anafariki dunia, Oktoba 14, 1999, Mwalimu Nyerere alikuwa msuluhishi wa kimataifa wa mgogoro wa Burundi na Rwanda, nafasi iliyochukuliwa baadaye na swahiba wake, Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela. Mwalimu leo anakumbukwa na mataifa mengi ya Afrika, kwa msimamo wake wa kupinga ubeberu, ukoloni na uonevu wa aina zote.
Kwa miaka mingi, alikuwa Mwenyekiti wa Nchi Zilizo Mstari wa Mbele Katika Ukombozi Kusini mwa Afrika. Aliifanya Dar es Salaam kuwa makao makuu ya harakati hizo. Wapigania uhuru kutoka Afrika Kusini, Angola, Msumbiji, Namibia, Zimbabwe na kwingineko, waliishi Tanzania na kupewa mbinu za kuondoa tawala dhalimu nchini mwao.
Mwalimu alikuwa anasema kwamba, hakuna maana kwa Tanzania kuwa huru, bila Afrika yote kujikomboa. Alisimamia, hadi wote wakakombolewa kwenye ukoloni na ubaguzi wa rangi. Makamanda na wapiganaji wa Tanzania walikwenda kushiriki katika mapigano ya kivita kwenye nchi hizo washirika, ili kuzipatia uhuru.
Ni Mwalimu, ni mtoto wa chifu, ni rais, ni mwenyekiti, lakini aliishi kimaskini, maisha ya kawaida, ya kujitolea, ya kujali wengine zaidi, ya kutoa kuliko kupokea. Hakika anastahili kuitwa mwana wa kweli wa Afrika. Tunapokumbuka leo kifo chake, hatuna budi kuyaenzi aliyotenda.
Mwalimu alichukua tabia ya watu kujirimbikizia mali kama ilivyo hivi sasa alikemea tabia ya viongozi wala rushwa, alikemea tabia ya viongozi walioendekeza udini na ukabila,mambo ambayo leo hii watanzania tunashuhudia hasa kuelekea uchaguzi mkuu.
Wakati wa mazishi ya mwalimu wapo baadhi ya viongozi walioapa kulinda rasilimali zetu lakini wao leo ndio warafi wakubwa na ndio wanaotafuna mali za walipa kodi.
Mwalimu aliona mbali na ndio maana hata alikataa madini yetu yasichimbwe leo hii nchi inaongozwa  na viongozi wenye tamaa ambao wamekuwa wakihubiri uongo kuwa wanamuenzi mwalimu kwa maneno wakati wanaihujumu nchi yetu.
Akiwa mtanzania mwenye uchungu na nchi yake aliona uchungu na ndipo alipoamua kuwa machimbo yetu yaachwe kwanza lakini leo tumeshuhudia migodi inavyotafunwa na wawekezaji wanatupa fadhila ya herikopta za kufanyia kampeni. Keki ya taifa inaliwa na wachache.
Leo hii ukifika butiama hutaamini kama kweli ndipo alipozaliwa muasisi wa taifa hili, serikali yetu imetekeza hata nyumba ya kwanza ya mwalimu aliyojenga alipotoka Tabora, hali ya maisha ya familia ya mwalimu inatisha lakini leo viongozi wanandai wanamuenzi mwalimu hivi kweli watanzania ni wepesi wa kusahau mema yote ya mwalimu kiasi hicho.
Wakati leo tunatimiza miaka 11 ya kifo chake watanzania lazima tujiulize mengi aliyotuachia mwalimu ambayo leo tunaona jinsi viongozi walioachiwa walivyoshindwa kuyatekeleza, na leo tena wanaomba ridhaa ya kuchaguliwa.
 
Hakika mwalimu alikuwa nuru ya wanyonge na mpenda haki  hakuna kiongozi atakayeweza kumfikia mwalimu kwa busara zake na maono yake, watanzania leo tumeachwa gizani hatujui tufanyeje.

Kwakweli kifo chake kiliacha masikitiko makubwa kwa Watanzania, Waafrika na hata nje ya bara letu hili, kikiwaacha wanyonge, kwa kuondokewa na mtu waliyempenda mno, aliyewajali na kuwasaidia kuifanya dunia kuwa mahali pazuri zaidi pa kuishi. Apumzike kwa amani. Amina.

No comments:

Post a Comment

Comments System

disqus

Disqus Shortname

msora

Popular Posts

Header Ads

ad