Sunday, September 23, 2012

Wahitimu kidato cha nne waaswa



NA Berensi Alikadi-Bunda

SERIKALI wilayani Bunda imewaasa wanafunzi waliohitimu elimu ya kidato cha nne kutobweteka na elimu waliyopata badala yake watambue kuwa bado wanalojukumu kubwa la kusonga mbele kielimu.

Kauri hiyo imetolewa jana na mkuu wa wilaya hiyo Joshua Mirumbe katika hotuba yake iliyosomwa na afisa mifugo na uvuvi wa wilaya hiyo,Masuke Ogwa kwenye mahafali ya sita ya shule ya sekondari ya Ellys iliyoko katika mamlaka ya mji mdogo wa Bunda.

Alisema kuwa pamoja na wanafunzi hao kufanya mahafali hayo lakini watambue kuwa kuna kazi kubwa ya mtihani ambayo wanapaswa kuifikilia kila siku katika maisha yao na akawataka kutumia muda mwingi katika kujiandaa na mtihani ambao utafanyika hivi karibuni nchini kote.

‘’Niwapongeze kwa kuhitimu leo lakini naomba msibweteke tambueni kuwa kazi kubwa bado iko mbele yenu huu ni mwanzo tu mtaenda vyuo vikuu na vyuo vingine nawaomba mjitahidi na muwe mabalozi wazuri kumbukeni bila elimu hakuna maisha hivyo jitahidini musome kwa bidii na muepukane na vitendo viovu’’alkisema Masuke.

Awali wakisoma risala ya kuhitimu masomo yao wanafunzi hao walisema kuwa walianza masomo yao mwaka 2009 wakiwa wanafunzi 215 ambapo wamehitimu wakiwa wanafunzi 175 na kwamba wanafunzi wengine wameshindwa kuhitimu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro na mamba na utovu wa nidhamu.

Akitaoa taarifa ya shule hiyo kwa wazazi,mkuu wa shule hiyo Mwalimu Feston Onanda alisema kuwa tangia kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 2005 imekuwa ikifanya vizuri katika mtihani ya kidato cha pili na cha nne ambapo hadi sasa zaidi ya wanafunzi 48 toka katika shule hiyo wamefanikiwa kujiunga katika vyuo vikuu na vyuo mbalimbali hapa nchini.

Alisema kuwa katika kuhakikisha kiwango cha elimu shuleni hapo kinapanda  shule hiyo imeweka mikakati ikiwa ni pamoja na kusimamia ufundishaji na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanatoa mazoezi ya mara kwa mara,kuhakikisha wanatoa mitihani ya kila wiki na kufauatilia mahudhulio ya wanafunzi ipasavyo.
Naye mkutugenzi wa shule hiyo Eliah John Maduhu alisema pamoja na mafanikio hayo bado kuna changamoto kubwa katika suala la elimu ambazo alizitaja kuwa baadhi ya wazazi kukosa ushirikiano na shule hivyo kufanya malezi ya wanafunzi kuwa mabaya,baadhi ya watoto kutoenda masomo na kufanya yao kutoridhisha.

Hata hivyo Maduhu aliomba serikali kuzisaidia shule binafsi kwa kuzipatia vifaa kama vile vitabu na vifaa vya maabara kwa masomo ya sayansi wakati wa mtihani kwani shule nyingi za binafsi hazipati vitabu na kuzingatia kuwa mitaala hubadirika siku kwa siku.

Mwisho


No comments:

Post a Comment

Comments System

disqus

Disqus Shortname

msora

Popular Posts

Header Ads

ad