
Majeshi Kismayo
Hatimaye wanajeshi wa AMISOM
wameuteka mji wa Kismayo.
Msemaji wa jeshi la Kenya Kanali Cyrus Oguna
aliambia BBC kuwa wanajeshi wa Kenya kwa ushirikiano na wale wa Somalia
walianza harakati zao mapema asubuhi ya leo.Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari, Luteni Generali Gutti alisema kuwa nia na lengo la wanajeshi hao ni kuwakomboa watu wa Kismayo na kuwawezesha kuishi kwa amani na usalama.
Alidokeza kuwa harakati zinaendelea kulenga maeneo ya Al Shabaab mjini humo.
Aliongeza kuwa angewataka wapiganaji waliosalia Kismayo kujisalimisha
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baadhi ya wapiganaji wa kundi hilo walio mjini humo, wameelezea nia yao kutaka kujisalimisha. Nayo AMISOM imewahikikishia usalama wao ikiwa wataweza kujisalimisha
Lakini mwandishi wa BBC anasema kuwa Al Shabaab husalimu amri kwa muda wakati wanapokabiliwa na majeshi yenye nguvu kuwaliko.
Ndege za kivita za Kenya zilifanya mashambulizi ya angani mapema wiki hii na kuharibu bohari lenye silaha za wapiganaji hao mjini humo.
Wiki iliyopita, Al Shabaab walijiandaa kuondoka Kismayo na hata kuwahamisha wapiganaji wao pamoja na silaha.
Mji huo wa bandarini ni muhimu kwa Al Shabaab kwani wanautumia kuingizia silaha na pia kuwatoza kodi wenyeji wa mji huo.
Hatua ya wao kupoteza mji huo, itakuwa ni pigo kubwa kwao, lakini wapiganaji hao wa Al Shabaab bado wana uwezo wa kufanya mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Somalia na wale wa Muungano wa Afrika hata katika sahamu ambazo wanajeshi hao wanadhibiti.